Habari mpya

USHAIRI: Cheka Ukinikumbuka

Banati wanivutia,kuaga ninaumia,
Tangu ninatia nia,hadi leo ninavyolia,
Na kwako nilitulia,ila umenikimbia,
Cheka ukinikumbuka,fukara mwenye mapenzi.
Tangu najiweka kwako,nilikuonesha penzi,
Nikakupa na cheko,kutishwa hata na panzi,
Leo niende huko,wanisukuma kwa konzi,
Cheka ukinikumbuka,fukara mwenye mapenzi.
Nilijitoa kwa heri,useme nini muhibu,
Leo watoka kwa shari,ni nini kimekusibu,
Eti tatizo ni gari,ya kale yamekusibu,
Cheka ukinikumbuka,fukara mwenye mapenzi.
Kweli ulinikomboa,kwenye nyakati za dhiki,
Ila leo waliona doa,Mori leo sibebeki,
Ama ni kunikomoa, na yule harudishiki,
Cheka ukinikumbuka,fukara mwenye mapenzi.
Ugomvi waleta kwangu,eti ni wale wale,
Ila namwachia Mungu,atanilipia kule,
Atanipoza machungu,na kufurahi milele,
Cheka ukinikumbuka fukara mwenye mapenzi.
Kaditama nagota hapa,nguvu zinaniishia,
Kwako nimetoka kapa,na moyo wautishia,
Mapenzi nayaogopa,kwa uliyonifanyia,
Cheka ukinikumbuka,fukara mwenye mapenzi.

No comments