WAZIRI MKUU ANAYETEMBELEA PIKIPIKI
JINA la N. Rangaswamy ni maarufu sana India, hii inatokana na ukweli kuwa huenda kwa sasa akawa ni mwanasiasa mwenye madaraka makubwa na aliye karibu zaidi na wananchi hasa maskini.
Rangaswamy ni waziri mkuu wa muungano wa majimbo ya Puducherry, nafasi ambayo amekuwa akiishika toka mwaka 2001 hadi 2008, kisha akaingia tena mapema mwaka huu hadi sasa.
Alizaliwa Agosti 4, 1950, na amejizolea umaarufu na heshima kubwa kutokana na msimamo wake katika kutetea haki za binadamu na za watu maskini.
Tangu akiwa mdogo amekuwa akijihusisha na siasa kama mfuasi wa Marehemu. K Kamaraj (rais wa zamani wa chama cha National Congress & CM la Tamil Nadu).
Anasifika kwa uaminifu. Amewahi kuwa Waziri wa Kilimo na Ushirikiano (1991), Waziri wa Kazi ya Umma na Kilimo (1996).
N Rangaswamy alichaguliwa kuwa waziri mkuu katika mwaka 2001 na tena mwaka 2006. Chini ya uongozi wake, eneo la Pondicherry alimekuwa likisifika kuwa ni lenye kufaa sana kwa kuishi kwa kuwa amekuwa mstari wa mbele kusaidia jamii na kurekebisha miundo mbinu. Amekuwa ni mwanasiasa aliyejizolea tuzo kadhaa zikiwemo za kutoka Marekani, akionekana kama mtu asiyejirimbikizia mali na mpenda haki kwa wananchi.
1991 - Thattanchavadi - Waziri wa Kilimo
1996 - Thattanchavadi - Waziri wa Walemavu
2000 - Thattanchavadi - Waziri wa Elimu
2001 - Thattanchavadi - Waziri Kiongozi
2006 - Thattanchavadi - Waziri Kiongozi
2011 - Kathirkamam na Indra Nagar - Waziri Kiongozi
Kama Waziri Mkuu
Rangaswamy anasifika sana kwa kuimarisha miundo mbinu eneo la muungano sambamba na maisha ya wananchi kwa ujumla.
Katika sekta ya elimu hali ni nzuri zaidi, kwani ameanzisha mpango wa elimu ya bure kwa wote, huku watoto wa shule za msingi wakipewa chakula kila wanapokwenda shule, hali ambayo imekuwa ikisababisha maskini wengi kukimbilia shule wakale.
Aidha wananchi wamekuwa karibu mno na uongozi wake kiasi kwamba maamuzi mengi makubwa ya kiutawala, wananchi wanahusishwa na kuulizwa kama wangependa kufanyike lipi au lini.
Rangaswamy anafahamika pia kama ni mwanasiasa mwenye msimamo mkali, kiasi kwamba huwa hapendi kuyumbishwa kwa lolote. Akiwa Waziri Mkuu wa eneo hilo, tarehe 28 Agosti 2008, wakati akiwa kwenye chama cha Congress, aliamua kujiulizuru.
Kwa kujiamini Januari 2011, alianzisha chama cha siasa iitwayo All India N.R Congress. Alikitangaza rasmi chama hicho 07, Februari 2011 katika ofisi ya makao makuu ya chama katika jengo liitwalo JJ Complex, Puducherry.
Kauli mbiu ya chama ni unyenyekevu, Haki na Uwazi. Ndani ya miezi mitatu ya uzinduzi wa chama, katika uchaguzi wa Bunge la 2011, alishinda na chama chake kikaingia madarakani kutawala eneo hilo. Ni ndani ya miezi mitatu tu tangu kuanzishwa, ndipo kuliitishwa uchaguzi, lakini katika uchaguzi wa majimbo mwaka 2011, chama chake kilipata viti 15 kati ya 17. Sababu kubwa ya kufanikiwa kwake katika siasa ni kuwa karibu na wananchi na kuwasaidia kweli.
Ingawa hakupenda kuwa na madaraka makubwa ndani ya chama, wengi waliendelea kumshawishi abaki kama kiongozi hasa kutokana na kumuamini kuwa ni kiongozi shupavu, mwenye kutoa maamuzi sahihi na asiyetishwa na chochote.
Anajulikana pia kwa ukarimu wake na nguvu ya kidiplomasia. Yeye anajulikana kama mtu wa watu, mwenye uwezo wa kuongea na yeyote, kwani wakati fulani amekuwa akitembelea watu maskini na kula nao.
Katika India, yeye ni waziri mkuu ambaye inaonekana ni kama hatishwi na chochote kwani hata hahofii usalama wake. Amekuwa akitembea wakati fulani na pikipiki mitaani na kusalimiana na watu anaowataka.
Mtu yeyote anaweza kuwasiliana nae, anaweza kuzungumza nae hata kama ni maskini sana, tajiri au wa chama chochote. Amewekewa ulinzi, lakini muda mwingi walinzi wake ni kama wanajikuta wana kazi kubwa ya kwendane nae, hasa anapoamua kuendesha pikipiki kutembelea sehemu anazotaka nk.
Nyumbani kwake amekuwa na kawaida ya kukutana na watu wa aina tofauti, mara nyingi kila asubuhi.
“Tunaona ni waziri mkuu wa aina yake ambaye milango yake imefunguka, wananchi tunayo nafasi ya kuongea naye tutakavyo,” anasema Srinivasa Kumar, mkazi wa Indore-India.
Wananchi wengi wa India, wanamuona Rangasamy kama ni mtu wa kufaa kuigwa na wanasiasa wengi wa India na Dunia kwa ujumla, kwani hawana matabaka.
Katika utafiti uliofanywa na jarida la India Leo` katika mwaka 2006, eneo analoongoza mwanasiasa huyo yaani Pondicherry lilishika nafasi ya kwanza kwa kutekelezwa kwa ahadi alizotoa wakati anaingia madarakani kwa vitendo.
Eneo hilo lilionekana kuwa ni zuri mno kuishi na kwamba kumekuwa na harakati nyingi za kusaidia jamii kuwa na maisha bora kwa India, kuliko eneo jingine lolote.
Baadhi ya mambo ambayo yanasifika sana kuendelezwa katika eneo hilo ni kuimarika kwa elimu, uwezeshaji wa wanawake, miundombinu, barabara, maji na demokrasia.
Yeye bado anaonekana kama ni Kamarajar aliye hai, mtu ambaye wengi pia walitokea kumsifia kwa namna ambavyo amekuwa karibu na wananchi katika kuwasikiliza na kuwasaidia ili wawe na maisha bora.
No comments