NMB Yaunganisha Bank Guarantee Kidijitali Kupitia NeST

Dar es Salaam, Machi 5, 2026 – Huduma ya uhakiki wa dhamana za zabuni za kibenki kupitia mfumo wa NeST imeelezwa kuwa hatua muhimu ya kuimarisha uwazi, ufanisi na usalama katika michakato ya ununuzi wa umma nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma ya uhakiki wa dhamana za zabuni za kibenki za Benki ya NMB kupitia mfumo wa NeST jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Bw. Denis Simba, alisema teknolojia hiyo itarahisisha michakato ya zabuni na kuondoa changamoto za uthibitishaji wa dhamana za kibenki.
“Kupitia mfumo wa NeST, taasisi nunuzi sasa zinaweza kuthibitisha dhamana za zabuni moja kwa moja kupitia mfumo bila kuwasiliana na benki husika, jambo ambalo linaongeza uwazi na ufanisi katika michakato ya ununuzi wa umma,” alisema.
Alieleza kuwa mzabuni ataweka namba ya dhamana aliyopewa na benki kwenye mfumo wa NeST, ambapo mfumo huo utaivuta moja kwa moja kutoka benki husika na kuiwasilisha kwa taasisi nunuzi kwa ajili ya uthibitishaji.

“Hatua hii imeondoa kabisa mianya ya kughushi nyaraka za dhamana za kibenki na pia inapunguza muda wa kuthibitisha uhalali wake,” alisisitiza.
Bw. Simba aliongeza kuwa matumizi ya teknolojia katika uthibitishaji wa dhamana za kifedha ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha mfumo wa ununuzi wa umma na kuongeza uwazi pamoja na usalama katika michakato ya zabuni na usimamizi wa mikataba.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, alisema kuunganishwa kwa mfumo wa NeST na mifumo ya benki hiyo kutasaidia kuboresha mfumo wa ununuzi wa umma na kuwawezesha wafanyabiashara kushiriki zabuni kwa uwazi na haki.
“Kupitia mfumo huu, NMB itawezesha uhakiki wa Bank Guarantee pamoja na akaunti za waombaji zabuni na kutoa majibu papo hapo, jambo litakalorahisisha mchakato na kuongeza ufanisi kwa wataalamu wa ununuzi na ugavi,” alisema.
Zaipuna alisema huduma hiyo ya kidijitali inalenga kupunguza matumizi ya karatasi, kuharakisha uthibitishaji wa dhamana na kuondoa hatari ya udanganyifu katika michakato ya zabuni.

“Kupitia huduma ya Digital Bank Guarantee Confirmation, wateja sasa wanaweza kuwasilisha na kuthibitisha dhamana za benki kama Bid Bond, Advance Guarantee na Performance Guarantee moja kwa moja kupitia mfumo wa NeST,” alisema.
Aliongeza kuwa hatua hiyo itapunguza muda wa kukamilisha taratibu za zabuni ambazo hapo awali zilikuwa zinachukua siku kadhaa.
“Kwa sasa NMB ni benki ya kwanza kuunganisha uthibitishaji wa Bank Guarantee kidijitali moja kwa moja na mfumo wa PPRA, hatua inayoongeza uwazi na ufanisi katika ununuzi wa umma,” alisema.
Aidha aliwahimiza wateja na wadau wanaotumia mfumo wa zamani wa dhamana za benki kuhamia mfumo huo mpya wa kidijitali ili kurahisisha ushiriki wao katika zabuni za serikali na kuongeza ufanisi katika shughuli zao za biashara.

No comments