Habari mpya

Benki Ya CRDB Kuwawezesha Wateja Wa ATCL Kufanya Malipo Ya Tiketi Kwa Urahisi


 

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kushoto) na  Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Denge la Tanzania (ATCL), Mhandisi Ladislaus Matindi wakionyesha ishara ya uzinduzi wa huduma ya malipo ya tiketi za ndege za ATCL kupitia mtandao wa Benki ya CRDB unaojumuisha matawi, CRDB Wakala na SimBanking katika hafla iliyofanyika leo jijini Arusha katika hoteli ya Mount Meru.

Benki ya CRDB imeingia ubia na Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kuwawezesha wateja wanaosafiri na ndege za shirika hilo kulipia tiketi za safari kupitia mtandao wa benki hiyo unaojumuisha Matawi 268 yanayopatikana nchi nzima, CRDB Wakala zaidi ya 20,000, pamoja na huduma ya SimBanking inayowezesha kufanya malipo kidijitali. 


Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba wa makubaliano iliyofanyika katika hoteli ya Mount Meru jijini Arusha, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema ubia huo na ATCL utasaidia kuhakikisha wateja wanafanya malipo kwa urahisi popote pale walipo nchini jambo litakalo saidia kuboresha huduma kwa wateja katika shirika hilo.


“Pamoja na kuwa wateja watakuwa wakilipia tiketi zao kwa urahisi, vilevile uunganishwaji wa mfumo huu wa malipo na mfumo wa ATCL utasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi katika upande wa upokeaji wa malipo ya tiketi. Tukiwa Benki ya kizalendo tunajivunia sana ubia huu na Shirika letu hili la ATCL ambalo pia ni la kizalendo,” amesema Nsekela.


Nsekela alibainisha kuwa hapo mwanzoni Benki hiyo ilikuwa ikiwawezesha wateja kulipia tiketi za ndege za ATCL kwa njia ya mtandao kupitia TemboCard, hivyo kuongezeka kwa njia hizo nyengine kunawapa wateja uhuru wa kufanya malipo kwa njia ambayo ni rahisi kwao kwa wakati husika. “Nawakaribisha wateja wote ambao wanasafiri na ndege za Shirika letu la ATCL kutumia njia hizi kufanya malipo kwani ni rahisi na salama, lakini wafanyakazi na CRDB Wakala wetu pia wapo tayari kuwahudumia,” aliongezea.


Naye Mkurungezi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Mhandisi, Ladislaus Matindi ameishukuru Benki ya CRDB kwa ushirikiano wa kibiashara ambapo Benki ya CRDB imekua benki ya kwanza kutoa huduma za benki kwa njia ya mtandao kwa shirika hilo ambalo kwa sasa linashikilia asilimia 75 ya soko la usafiri wa anga hapa nchini. Aidha amesema kuunganishwa kwa mifumo ya malipo ya Benki ya CRDB kunaendana na mikakati ya ukuaji wa shirika hilo ambapo hivi karibuni limeongeza safari za ndege ndani na nje ya nchi.


“Kama mnavyofahamu shirika letu limekuwa na mkakati wa kufika katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa kurahisisha safari za ndege ambapo hivi karibuni shirika hilo linatarajiwa kutanua wigo wa safari za nje ambapo safari za kuelekea Nigeria, Afrika ya Kusini, China na Uingereza zinatarajiwa kuanza hivi karibuni. Mkakati huu wa upanuzi wa biashara unaenda sambamba na kuhakikisha wateja wetu wanaweza kupata huduma bora popote pale walipo. Ni imani ushirikiano huu na Benki ya CRDB utasaidia kufikia azma yetu ya kutoa huduma bora za usafiri kwa njia ya anga,” amesema Matindi.


Akizungumzia namna ya kunua na tiketi na kufanya malipo kupitia mtandao wa Benki ya CRDB, Matindi alisema wateja watafuata hatua ya kawaida ya kuhifadhi wa tiketi kwa kutembelea tovuti ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) www.airtanzania.co.tz au Ofisi ya Mawakala kwaajili ya ambapo atapewa namba  ya uhifadhi wa tiketi (PNR) ambayo utaitumia kulipia tiketi iliyohifadhiwa kupitia mifumo ya Benki ya CRDB.


“Ikiwa mteja atatembelea kwenye tawi la Benki ya CRDB au CRDB Wakala ataonyesha namba yake ya uhifadhi tiketi na kisha kulipa kiasi husika kutokana na safari yake. Kwa upande wa SimBanking mteja baada ya kupata namba ya uhifadhi wa tiketi ataingia kwenye menu na kuchagua malipo kisha atachagua shirika la ndege la ATCL, ataingiza namba ya uhifadhi na kisha kufanya malipo,” amesema Matindi.


Hivi karibuni Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limeongeza safari zake za ndani na nje ya Tanzania ikiwa ni kipindi kifupi baada ya ujio wa ndege mbili aina ya Airbus, ambazo zimepelekea kuongezeka kwa safari mpya zilizoanza Novemba, 2021. Safari zilizoongezwa ni pamoja na Dodoma-Mwanza, Dar-Mtwara, Dar-Nairobi, Dar-Ndola Dar-Bujumbura ambapo Benki ya CRDB ina kampuni tanzu, pamoja na Dar-Lumbumbashi ambapo Benki hiyo ipo mbioni kufungua kampuni tanzu.

No comments