Dar es Salaam, 25 Oktoba, 2021 - Waziri wa Fedha na Mipango Dokta Mwigulu Nchemba amepokea gawio la shilingi bilioni 25 linalotokana na uwekezaji wa Serikali ndani ya Benki ya CRDB kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay.
Makabidhiano hayo ya hundi kifani yalifanyika katika Makao Makuu ya Benki ya CRDB yaliyopo Palm Beach jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa taasisi na mashirika ya umma yenye hisa ndani ya Benki ya CRDB na Menejementi ya Benki ya CRDB.
Akizungumza katika hafla hiyo Dkt. Nchemba aliipongeza Benki hiyo kwa kutoa gawio kwa Serikali, Dokta Nchemba aliipongeza Benki ya CRDB kwa kupata matokeo mazuri ya fedha mwaka 2020 ambayo yamepelekea kuongezeka kwa gawio kwa Wanahisa ikiwamo Serikali.
“Ongezeko hili la gawio ni kiashiria tosha kwa Serikali kuwa Benki yetu ya CRDB inazidi kuimarika zaidi kutokana na mikakati madhubuti ya kibiashara iliyojiwekea na jambo linalowapa moyo Watanzania na wawekezaji kuwa benki inatoa huduma bora katika jamii”, alisema Dkt. Nchemba.
Dkt. Nchemba alisema fedha zilizopatikana kupitia gawio hilo zitakwenda kusaidia utekelezaji wa miradi ambayo Serikali imeianisha katika vipaumbele vya bajeti ya mwaka 2021/2022 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa 2021/22 - 2025/26 hususan katika sekta ya afya. “Kipekee kabisa niipongeze Bodi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Benki ya CRDB kwa kazi nzuri mnayoifanya ambayo imepelekea kupatikana kwa gawio hili nono,” aliongezea Dkt. Nchemba.
Aidha, Dokta Nchemba aliipongeza Benki ya CRDB kwa matokeo mazuri ya fedha iliyopata katika nusu ya kwanza ya mwaka huu 2021 ambapo faida ya Benki imeongezeka kwa asilimia 26 kufikia shilingi bilioni 89 kutoka TZS bilioni 70.4 zilizoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2020. “Mkiendelea na kasi hii mwakani tunategemea kupata gawio nono zaidi,” alisema Dokta Nchemba.
Dokta Nchemba alipongeza jitihada mbalimbali za Benki ya CRDB katika kuchangia maendeleo ya Taifa ikiwamo ulipaji wa kodi ambapo mwaka jana ililipa jumla ya kodi ya shilingi bilioni 181.4. Alipongeza pia jitihada katika utoaji wa ajira kwa vijana na uwezeshaji kupitia Sera ya Kusaidia Jamii (CSR Policy). “Nimevutiwa sana na mkakati wa Benki ya CRDB katika kusaidia kutoa ajira kwa vijana kupitia program ya mafunzo kazini ‘internship’ na mafunzo kwa wahitimu ‘graduate development program.”
Akizungumzia mikakati ya Serikali katika kuimarisha sekta ya fedha, Dkt. Nchemba alisema mwaka huu Serikali imechukua hatua mbalimbali za kusaidia kuiboresha sekta hiyo ikiwamo kupunguza kiwango cha amana za mabenki Benki Kuu, kuanzishwa kwa mfuko wa kukopesha taasisi za fedha, na kupunguza kiwango cha mtaji kinachotakiwa kwa ajili ya kuweza kutoa mikopo zaidi kwa sekta binafsi.
Kwaupande wake Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Mette Dissing-Spandet alisema Denmark inajivunia uwekezaji wake kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia DANIDA ndani ya Benki ya CRDB. Alisema matokeo mazuri ya kifedha ambayo benki hiyo imekuwa ikiyapata yanaonyesha ni jinsi gani benki hiyo inatoa bidhaa na huduma bunifu na zinazoendana na mahitaji halisi ya wateja.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay alisema kuwa gawio ambalo limekabidhiwa leo hii ni sehemu ya faida ya shilingi bilioni 165.2 baada ya kodi ambayo Benki ya CRDB na kampuni zake tanzu imeipata katika mwaka wa fedha 2020. Pia ameeleza kuwa Benki hiyo itaendelea kutoa huduma bora ili kukidhi mahitaji ya wanahisa wake na wananchi kwa ujumla.
“Katika Mkutano wa Wanahisa uliofanyika kidijitali mwezi Juni mwaka huu, Wanahisa wa Benki ya CRDB walipitisha kwa pamoja gawio la shilingi 22 kwa hisa ikiwa ni ongezeko la asilimia 37.5 na hivyo kufanya gawio la mwaka huu kufikia shilingi bilioni 58,” aliongezea Dkt. Laay.
Aidha, Dkt. Laay alipongeza jitihada za Serikali za kuendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara nchini ambazo alisema ndio zimesaidia kuiwezesha Benki ya CRDB kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na kuahidi kuendelea kushirikiana nayo ili kukuza uchumi wa nchi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela alimhakikishia Dokta Mpango kuwa Benki ya CRDB kupitia kauli mbiu yake ya “Tupo Tayari” itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha nchini huku akielezea kuwa benki hiyo sasa hivi imejikita zaidi kwenye uwekezaji wa mifumo ya kidijitali ya kutolea huduma kama CRDB Wakala, SimBanking na Internet banking.
Pamoja na kukabidhi gawio kwa Serikali kuu kupitia mfuko wa uwekezaji wa DANIDA, Benki ya CRDB pia imekabidhi gawio kwa taasisi na mashirika mbalimbali ya Serikali ikiwamo PSSSF, NSSF, ZSSF, NHIF, Local Government Loans Board, Chama cha Ushirika cha Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU), Umoja Unit Trust Scheme, TCCIA Investment Company Ltd, pamoja na halmashauri Mbinga, Shinyanga, Mufindi, Chunya na Rungwe.
Serikali ndio mwanahisa mkubwa ndani ya Benki ya CRDB kutokana na kuwa na umiliki wa asilimia 21 kupitia mfuko wa uwekezaji wa DANIDA kushirikiana na Serikali ya Denmark, huku taasisi na mashirika ya umma yakiwa na umiliki wa hisa za asilimia 17.1.
No comments