Habari mpya

Makadirio ya bajeti Kenya,Tanzania na Uganda yakamilika


Nchini kenya waziri wa fedha Henry Rotich leo amewasilisha bungeni bajeti ya makadirio ya matumizi ya pesa za serikali katika kipindi cha mwaka 2016-2017.
Bajeti hiyo ya jumla ya shilingi trilioni 2.26 inatarajiwa kufadhiliwa kupitia ukusanyaji wa ushuru na mikopo kutoka kwa washirika wa kimaendeleo. Serikali inalenga kukopa shilingi bilioni 778 hatua ambayo itaongeza deni la kenya ambalo kufikia sasa ni shilingi trilioni 3.32.
Matumizi zaidi itaelekezwa kwa ujenzi wa miundo mbinu ikiwa ni pamoja ujenzi wa reli ya kisasa, kuimarisha usalama, huduma za afya na pia kuziwezesha serikali za majimbo.
Kama ilivyo ada bajeti inaposomwa kuna wale wa wanaofaidi na wale wanaopoteza. Gesi ya kupikia na chakula cha mifugo umeondolewa ushuru, Huku ushuru wa petroli na mafuta taa ukiongezwa. Bidhaa za mafuta ya urembo zikiwekewa ushuru wa asilimia kumi kwa mara ya kwanza.
Waziri ametenga shilingi bilioni 4.3 kwa huduma za bure za wanawake wajawazito kujifungua,milioni 19.7 kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 na shilingi milioni 7.9 kwa watoto mayatima.


Nchini Tanzania makadirio ya bajeti ya mwaka 2016 na 2017 ni trilioni 29,5 pesa za Tanzania ikiizidi bajeti ya mwaka wa 2015 na 2016 kwa trilioni 7.1.
Waziri wa Fedha nchini Tanzania Phillip Mpango alisema kuwa kati ya fedha hizo, Shilingi trilioni 18.46 zitatokana na jumla ya mapato ya ndani.
Kiwango hicho kimezidi shilingi trilioni 3.64 za bajeti iliyopita ambayo ililenga kukusanya shilingi trilioni 4.82.
Shilingi trilioni 17.72 zitakuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, huku trilioni 11.82 sawa na asilimia 40 ya bajeti nzima, zikitengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Bwana Mpango alisema washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia shilingi trilioni 3.6, ikiwa ni ongezeko la shilingi trilioni 1.7 ikilinganishwa na shilingi trilioni 1.88 zilizokuwa zinategemewa kwenye bajeti iliyopita.
Makadirio ya bajeti nchini Uganda mwaka 2016 na 2017 iliyosomwa leo ni ya jumla ya dola bilion 7.5 ambayo ni sawa na trillioni 27. 3 pesa za Uganda, tofauti na bajeti ya mwaka uliopita ya mwaka 2015 na 2016 ambayo ilikuwa ni dola bilioni 6.9.
Bajei kubwa mwaka huu nchini Uganda imeelekezwa kwa wizara ya kazi na uchukuzi ambayo ilipewa dola blioni 1.1 huku wizara ya ulinzia ikipewa dola milioni 435. Wizara ya afya imepata dola milioni 525.
Wizara ya nishati na maendeleo ya madini ilipata dola milioni 695 huku Wizara ya kilimo ambayo nidiyo muhimu nchi Uganda ikiewa dola milioni 522.

No comments