Habari mpya

HISTORIA YA SANAMU LA MLINZI (POSTA)

 Sanamu (5)
Historia ya Mnara ule ilianza mwaka 1889, kisha, kabla na baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia (1914 - 1918) hadi Vita Kuu ya Pili ya Dunia (1939 - 1945).
Kwa ufupi Sanamu ya mwanzo kukaa pale ni sanamu ya Herman Von Wissman, Gavana wa Kijerumani ambaye anakumbukwa kwa kutekeleza utekaji na mauaji ya Abushir Ibn Salim Al Harthi, mtawala/sultani
wa Pangani Tanga.

Baada ya kumteka na kumyonga Abushir, Von Wissman alirejea Ujerumani na kisha baadaye kuteuliwa kuwa Gavana wa Nchi zilizokuwa chini ya Ujerumani za Afrika Mashariki (German East Africa). Alitwaa Dar es Salaam na Pwani nzima, japo alikaa muda mchache Dar es Salaam.
Gavana huyu alifanya utafiti wa kutafuta ni wapi kitovu cha mji wa mji wa Dar es Salaam. Yaani katikati mwa mji kwa vipimo, ndipo alipogundua eneo lile pale Posta na kisha akaagiza pajengwe bustani na Sanamu lake likasimikwa. Inadaiwa pale ndipo palikuwa katikati mwa Dar es Salaam miaka ile.
Inaaminika ndiye aliyetoa wazo la kutengeneza ramani ya kujenga makambi ya wapiganaji ama wanajeshi wa Jeshi la Ujerumani eneo ambalo lilikuwa likiitwa Carrier Corps (Waswahili wakaita Keriakoo/Kariakoo). Ndio maana utaona mitaa ya Kariakoo imenyooka na kujengeka vizuri. Ilikuwa makambi ya wanajeshi.
Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia iliyopiganwa kuanzia mwaka 1914 hadi 1918 ambapo Waingereza walishinda na kuchukuwa koloni la Tanganyika, mwaka 1916 ndipo Sanamu la Bwana Herman Von Wissman liliondolewa na likawekwa Sanamu la sura ya Askari Mweusi mwaka 1927 kama ishara ya kuthamini mchango wa Askari Waafrika waliopigana kwenye Vita hivyo. Lile Sanamu limedumu hadi leo hapo panapoitwa Askari Monument.
Hiyo ni historia fupi. Yule Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Ulanga Mashariki ilibidi arejee kidogo kwenye historia hii fupi kabla ya kupendekeza kuondoa kwa Sanamu ile na kuweka sanamu ya Diamond. Sanamu ile ina uzito katika Historia ya nchi hii na bado inahitajika kuenziwa na kuhifadhiwa kwa Historia ya Vizazi vijavyo....

No comments