TIGO YAMDHAMINI MWANAMUZIKI BEN POL KUBURUDISHA TAMASHA LA NYAMA CHOMA
Mkuu wa Kitengo cha Burudani na Digitali wa Tigo, Paulina Shao (kushoto), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo kuhusu tamasha la nyama choma litakalofanyika Viwanja vya Leaders kesho kutwa Jumamosi Mei 28, 2016 jijini Dar es Salaam, ambapo mwanamuziki Ben Pol atatoa burudani kwa udhamini wa kampuni ya Tigo. Kulia ni Mratibu Mkuu wa Tamasha hilo, Carol Ndosi na katikati ni mwanamuziki Ben Pol.
Mratibu Mkuu wa Tamasha hilo, Carol Ndosi (kulia), akizungumza katika mkutano huo.
Mwanamuziki, Ben Pol (katikati), akizungumza katika mkutano huo.
Mtaalamu wa Kidigitali, Samira Baamar (kushoto), akichangia jambo kwenye mkutano huo.
Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali wakichukua taarifa hiyo.
Na Dotto Mwaibale
Kampuni inayooongoza kwa maisha ya kidijitali Tigo Tanzania leo imekubali kumdhamini mwanamuziki nguli na mtunzi wa nyimbo za muziki, Bernard Michael Paul Mnyang'anga, maarufu kama ‘Ben Pol’ kuburudisha katika tamasha la mwaka huu la Nyama Choma.
Tamasha hilo ambalo linafanyika kwa mwaka wa tano sasa ni moja ya tamasha maarufu linalovutia watu wengi kutoka maeneo yote ya Dar es Salaam litafanyika kwenye viwanja vya Leaders Jumamosi Mei 28, 2016.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, Mkuu wa Tigo wa masuala ya Dijitali Paulina Shao alisema kuwa kumuunga mkono Ben Pol kunaonesha kuendelea kujikita kwa Tigo katika kuwekeza katika kusaidia sekta ya muziki ya ndani kwa kuhakikisha wasanii wanawezeshwa kufikia viwango vya juu katika kazi zao.
“Kama kampuni ya maisha ya kidijitali, Tigo inatambua mchango muhimu wa wasanii wa Tanzania wanaoutoa katika sekta ya burudani.
Hii ndio maana tumewekeza kwa kiwango kikubwa kuwasaidia wasanii hususani wanamuziki wa ndani katika kuhakikisha wanafahamika katika masoko ndani ya nchi, kikanda na kimataifa kwa kutumia majukwaa ya kidijitali yanayokuwepo na kushiriki matukio mbalimbali na hivyo kuongeza mauzo ya muziki wao pamoja na nembo zao,” alisema Shao.
Aidha akiishukuru Tigo kwa uungwaji mkono huo, Ben Pol aliisifu Tigo kwa juhudi inazofanya bila kuchoka katika kukuza ukuaji wa sekta ya muziki wa ndani kupitia Jukwaa la Muziki la Tigo.
“Ninaishukuru sana Tigo kwa uungwaji mkono ambao ni muendelezo wa mtiririko wa programu ambazo imezianzisha ili kuinua maisha ya wasanii wachanga wa Tanzania,” alisema Ben Pol na kutoa changamoto kwa wasanii wanaoibukia kuwa wasione aibu kuomba msaada kutoka kwa mashirika kama Tigo.
Nguli huyo wa muziki wa Bongo Flava kwa hivi sasa anatamba na kibao ‘MoyoMashine’ ambayo aliitoka hivi karibuni.
Ben Pol ni miongoni mwa wasanii wanaonufaika na jukwaa la Muziki la Tigo ambalo lilianzishwa mwaka 2015 likiwa na lengo la kuiunga mkono sekta ya muziki Tanzania kwa kuwasaidia wasanii wa ndani kupata kipato zaidi kutokana na mauzo ya kazi zao na kuwawezesha kufahamika katika masoko ya kimataifa kupitia majukwaa hayo ya kidijitali kama vile Music portal na Deezer, ambayo ni majukwaa ya kimataifa yaliyo kwenye mtandao yakiwa na nyimbo kutoka sehemu mbalimbali duniani zaidi ya milioni 36.
No comments