SIRI IMEFICHUKA, KAZI NJE NJE. SOMA HAPA UJIPATIE KAZI.
Kupata nafasi za ajira imekuwa ngumu siku hadi siku, hususani ukitilia maanani kuwa wahitimu wanazidi kuwa wengi na hali ngumu ya uchumi inafanya waajiri kushindwa kuongeza nafasi mpya za kazi. Hauna haja ya kukata tamaa ya kupata kazi ile unayoitarajia hata kama kuna ukiritimba mwingi katika soko la ajira kama vile watu kupeana kazi kwa kujuana, nafasi za kazi kutotangazwa au kazi haipatikani mpaka rushwa itembee. Makala hii inaenda kujadili mambo ya msingi kwa yeyote anayetafuta kazi, uwe kwa sasa umeajiriwa unatafuta kazi mbadala au uwe hauna ajira unatafuta ajira, bila shaka mambo tunayojadili hapa yatakusaidia.
1.Mtazamo wako kuhusu ajira:
Fahamu
kuwa bidhaa ni chochote kile ambacho
kinatimiza mahitaji fulani. Mwenye kuhitaji bidhaa huwa tunamuita mteja. Muajiri anatafuta mfanyakazi kwa kuwa analo
hitaji la kazi fulani kukamilika, na anayo matarajio kadhaa toka kwa mfanyakazi
anayemuajiri. Hivyo wewe kama
mfanyakazi mtarajiwa unayo ‘bidhaa’, yaani uwezo wako wa kutimiza majukumu
fulani ambayo utatakiwa kufanya na muajiri. Kwahiyo mtazamo sahihi unaotakiwa
kuwa nao wakati unatafuta kazi ni kuwa wewe ni muuzaji wa bidhaa, na muajiri wako mtarajiwa ni mteja.
Kwakuwa wapo ‘wafanyabiashara’ wengi wa hiyo bidhaa kama yako (watu
wanaotafuta ajira), unahitajika basi kujipanga vema ili kumshawishi na kumfanya
mteja wako (muajiri mtarajiwa) aone
kweli sababu ya kununua ‘bidhaa ‘toka kwako.
2.Wasifu wako ujitosheleze:
Ukiwa
na mtazamo tuliouleza hapo juu wa kuwa wewe ni mfanyabiashara unauza bidhaa kwa
mteja wako (muajiri), unatakiwa basi utumie vema wasifu wako (CV) kujieleza
vema ili ‘mteja’ akukubali.Mambo ya kuzingatia katika wasifu wako ni kama
yafuatavyo:-
- Wasifu wako uendane na aina ya kazi unayo omba: Hivyo basi usiweke kila aina ya maelezo hata yale ambayo haya umuhimu na kazi husika. Mfano unaomba nafasi ya kazi ya uhasibu, lakini unaweka maelezo ya uzoefu wa sehemu tatu tofauti ya kazi za ulinzi.
- Wasifu wako uonyeshe kweli unao uwezo wa kazi unayoiomba: Hivyo basi usitaje tuu majina ya kampuni au asasi ulizofanya kazi na aina ya cheo ulichoshika ukiwa huko, bali eleza mambo ya msingi ambayo ni mafanikio ya wewe kuwepo katika kampuni au asasi fulani uliyokuwepo. Mfano kwa kazi yako kama msimamizi wa ofisi, uliweza andaa mikutano (itaje) ambayo ilikutanisha watendaji wakubwa wa kampuni yako ambapo kupitia maandalizi mazuri uliyoyafanya, kampuni yako iliweza kupendekezwa mara tatu mfulululizo kuandaa mikutano hiyo.
- Wasifu wako uonyeshe utofauti wako wewe na watu wengine: Haitoshi kuandika katika CV yako kuwa umemaliza masomo ya ngazi ya stashahada au shahada, haitoshi kutaja kuwa umewahi kufanya kazi fulani mfano kazi ya usimamizi wa ofisi halafu ukaorodhesha majukumu ya msimamizi wa ofisi, mambo ambayo kwa ujumla yanajulikana kuwa ni majukumu ya msimamizi wa ofisi yeyote yule wa ofisi. Kumbuka wasifu wako (CV) ni nyaraka muhimu ya kumshawishi ‘mteja’ kuwa ananunua ‘bidhaa bora zaidi ya nyingine katika soko la ajira. Hivyo basi jipange kwa kuonyesha utofauti, badala ya kutaja tuu ngazi za juu za elimu ulizofanikiwa kufika, taja pia maeneo ambayo wewe kweli ‘upo mzuri’ yaani maeneo ambayo kweli haubabaishi katika ngazi hizo za elimu unazotaja. Pia kwa upande wa uzoefu wa kazi, taja mafanikio uliyokwisha pata kutoka ajira zako zilizopita, au tuseme mambo gani ‘mazito’ ulikamilisha na kusaidia ukiwa kwa waajiri wengine.
3. Fuata maelekezo kwa ufasaha:
Unapowasilisha
maombi yako ya ajira, hakikisha unafuata maelekezo yaliyotolewa katika tangazo
la nafasi za kazi, kwani hata kama ni jambo dogo, utakalokosea linaweza
kuchukuliwa kama sababu ya wewe kutokuwa mfanyakazi makini, hivyo kukosa hata
nafasi ya kuitwa kwa usaili (interview). Mfano kama umeambiwa uorodheshe
wadhamini watatu, hauna sababu ya kuorodhesha wadhamini wawili tuu. Kama
umeambiwa utume maombi kwa njia ya posta, usitume maombi yako kwa barua pepe
wala kupeleka kwa mkono.Hakikisha pia unafuata maelekezo ya tarehe na muda wa
kuwasilisha maombi yako ya kazi. Pia zingatia maelekezo kuhusu vyeti na nyaraka
nyingine unazotakiwa kuziambatanisha pamoja na barua yako ya maombi ya kazi.
Kama umeambiwa utume CV yako tuu, usihangaike kutuma vitu vingine kama vyeti,
na barua ya maombi ya kazi.
4.Barua ya maombi ibebe uzito:
Barua
yako ya maombi ya kazi ni nafasi nyingine ya kushawishi ‘wateja’ wako kuwa kweli
utawapatia huduma wanayoitaka, na kwamba watakapofanya chaguo la kukuajiri wewe
watakuwa wamefanya chaguo bora kabisa. Anza kwa kueleza aina ya kazi unayoomba,
umetambuaje uwepo wa nafasi hiyo ya kazi. Jieleze kwanini wewe ni chaguo lao
bora kwa kulinganisha majukumu ya kazi unayoomba na ujuzi wako, uzoefu wako, na
yale uliyokwisha wahi kufanikisha hapo kabla.
Kwakuwa barua ya maombi ya kazi huwa ni fupi, usiwachoshe kwa maelezo
mengi, ila maelezo yako yawavutie kusoma nyaraka ulizoambatanisha kama vile CV
na vyeti .
5. Jiandae kwa ‘interview’:
Utakapopata
nafasi ya kuitwa kwa usaili, usiende bila kujiandaa. Fahamu vema majukumu
yanayoendana na nafasi ya kazi uliyoomba, hakikisha unakumbuka nini uliandika
katika barua yako ya maombi ya kazi na CV yako. Jikumbushe mambo ya msingi
kuhusu elimu ya darasani ambayo umetaja unayo. Jifunze pia maswali mbalimbali
ya kisaikolojia yaulizwayo katika usaili , kama vile ‘Tuambie madhaifu yako ni
yapi ?”. Unaweza jifunza jinsi ya kujibu maswali kama hayo kupitia vitabu au
hata kwa ku search kwa mtandao.
6. Usisubiri nafasi za kazi zikufuate:
Amini
kuwa kuna waajiri wengi ambao hawatangazi nafasi za kazi kwenye vyombo vya
habari au mitandaoni. Pia wapo ambao wamekwisha tangaza lakini hawajapata watu
wenye kukidhi kweli viwango vyao. Hivyo usingoje nafasi za ajira zikufuate kwa
kupitia vyombo vya habari, badala yake wewe mwenyewe wasiliana na waajiri
mbalimbali ukiwaeleza nia yako na uwezo wako wa kufanya kazi kwao. Waweza tembelea ofisi za makampuni au asasi
mbalimbali na pia tembelea website na
hata maonyesho ya biashara au maonyesho ya waajiri (Job Fairs). Njia nyingine
ni kujenga mitandao na watu mbalimbali ambapo kupitia mitandao hiyo waweza
jieleza hitaji lako la kutaka ajira. Kumbuka kama una ‘bidhaa’ bora, na
ukimpata mteja mwenye kuhitaji ‘bidhaa’, bila shaka una nafasi kubwa ya kupata
ajira.
7. Itunze ‘taswira’ yako:
Waajiri
wengi hupenda kufahamu zaidi kuhusu mtu wanayetaka kumuajiri, sio tuu uwezo
wake kiujuzi wa kazi, bali pia uaminifu wako, wewe ni mtu wa aina gani katika
kujiheshimu na kujiheshimu wengine n.k. Hivyo hakikisha hauharibu ‘taswira’
yako kupitia aina ya marafiki ulionao, aina ya twitts, status, picha n.k unazoweka
katika mitandao ya kijamii kama Facebook, na Twitter. Pia unapotaka kuacha kazi
toka asasi fulani , jitahidi uache kwa amani, isije baadae waajiri wako wengine
wakataka kujua aina gani ya mfanyakazi ulikuwa hapo kabla wakajibiwa habari
isiyopendeza.
No comments