Home
/
Daniel Burton Mwaseba
/
KABLA HAUJAANZA KUZUNGUKA NA NA BAHASHA YENYE CV NA VYETI ILI KUFUKUZIA AJIRA PATA ELIMU YA BURE
KABLA HAUJAANZA KUZUNGUKA NA NA BAHASHA YENYE CV NA VYETI ILI KUFUKUZIA AJIRA PATA ELIMU YA BURE
Kuna uwezekano umeshaandaa vyeti vyako na wasifu wako na upo kwenye
michakato ya kuanza kuzunguka na bahasha kupeleka sehemu mbalimbali ii
kuomba nafasi ya ajira. Kabla hujaweka nguvu na matumaini yako kwenye
mchakato wa kuzunguka na bahasha kuna vitu vichache ambavyo ni vyema
ukavijua.
1. Nafasi za ajira ni chache kuliko idadi ya wahitimu
na wenye sifa. Kwa sasa karibu kila kada ukiondoa elimu na afya kuna
nafasi chache sana serikalini na hata kwenye taasisi binafsi. Hata kwa
kada ya elimu nako kwa miaka ya hivi karibuni kuna baadhi ya wahitimu
wamekosa nafasi za kazi. Hivyo unavyoingia sokoni jua kabisa ‘demand’ ni
ndogo kuliko ‘supply’
2. Sio kila nafasi za kazi
zinazotangazwa ziko wazi. Kuna baadhi ya taasisi zinatangaza nafasi za
kazi ili tu kutimiza wajibu na sheria ya kutaka ajira zitangazwe kwa
umma. Hivyo unaweza kuandika maombi, ukaitwa kwenye usaili na bado
ukaambiwa umekosa nafasi.
3. Wenzako wa mwaka jana na mwaka
juzi bado wanazunguka na bahasha. Bado kuna wahitimu wengi wa miaka
iliyopita nao bado hawajapata ajira. Kuna ambao bado wanaendelea
kupitisha bahasha na kuna baadhi ambao wameamua kufanya mambo mengine.
ni vyema kuwatafuta wa kila kundi ili ujifunze machache kutoka kwao.
4. Mishahara ya kazi za kwenye taasisi binafsi ni midogo sana. Tofauti
na story za vyuoni kwamba mishahara inaanzia labda laki tano au laki
saba jua kuna wenzako wana degree hivyo hivyo na wanalipwa laki mbili.
Kama ukipata kazi na mshahara wakakutajia mdogo kama huna kingine cha
kufanya ni bora kuchukua kazi hiyo ila uifanye kwa lengo la kupata ujuzi
na kujenga mtandao na watu wanaofanya kada uliyosomea. Kuliko kukaa
mwaka mzima ukizunguka na bahasha ukitegemea mshahara mkubwa ni bora
kupata japo laki mbili kwa mwezi huku ukiendelea kukuza mtandao wako na
ujuzi wako.
5. Kuna kazi za kujitolea, kama umekosa hata kazi
ya bei rahisi kuna taasisi nyingi ambazo zina mpango wa watu kujitolea
kufanya kazi na baadae unaweza kuingizwa kwenye ajira. Kama hali ya
nyumbani inaruhusu kwa kuweza kupata kula na nauli fanya kazi za
kujitolea na huko onesha uwezo wako na vipaji vyako. Kwa kuonesha uwezo
na vipaji ni rahisi sana kukubalika na kupewa nafasi, na pia
utatengeneza mtandao wa watu watakaokuonesha njia zaidi.
6. Sio
lazima ufanye kazi ya kitu ulichosomea. Kuna baadhi ya kazi zinaweza
kufanywa na mtu yeyote aliehitimu elimu fulani. Kwa mfano kwa sasa kuna
uhaba mkubwa wa walimu, hivyo kama umehitimu unaweza kutafuta shule na
ukafundisha masomo yanayohusiana na ulichosomea. Kama umesoma kada za
biashara unaweza kufundisha masomo ya biashara, kama umesoma sayansi
kuna nafasi kubwa za kufundisha masomo ya sayansi kutokana na uhaba wa
waalimu wa sayansi. Kama unadhani kushika chaki sio hadhi yako basi
endelea kuzunguka na bahasha mjini.
7. Angalia mazingira
yanayokuzunguka na jinsi unavyoweza kuyatumia kutengeneza ajira kwako na
kwa wanaokuzunguka. Hii ndio dhana halisi ya elimu ila kwa kuwa elimu
yetu inatuandaa kuwa waajiriwa basi tunajikuta wote tunasubiri
kuajiriwa.Ni vyema ukaanza kufikiri tofauti na uliyofundishwa chuoni
kuhusu ajira.
8. Cha mwisho kabisa ambacho ni vyema ukakijua na
ambacho ingebidi kiwe cha kwanza ni kufanya maamuzi ya kujiajiri. Kama
utachoshwa na kuzungusha bahasha ama kama hutaki kupata hiyo karaha ni
vyema ukafanya maamuzi ya kutotegemea kuajiriwa. Tumia uwezo na vipaji
ulivyonavyo changanya na elimu uliyoipata halafu tumia mazingira uliyopo
kutengeneza ajira kwako na kwa wanaokuzunguka.
KABLA HAUJAANZA KUZUNGUKA NA NA BAHASHA YENYE CV NA VYETI ILI KUFUKUZIA AJIRA PATA ELIMU YA BURE
Reviewed by Unknown
on
7:30 AM
Rating: 5
No comments